Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jeshi la Yemen lilitangaza kuwa limelenga Uwanja wa Ndege wa Abha kwa makombora ya balestiki na pia kutangaza marufuku ya safari za ndege katika anga ya Saudi Arabia. Hatua hiyo imezua mjadala mpana katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii, Jeshi la Yemen lilieleza kuwa operesheni hiyo ni jibu la shambulio la hivi karibuni ya Saudi Arabia dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a.
Wanaharakati, wanasiasa na vyombo vya habari wanaamini kuwa hatua hiyo inaashiria kuanza kwa awamu mpya ya mkakati wa kuzuia mashambulizi, unaojengwa juu ya kaulimbiu ya "uwanja wa ndege kwa uwanja wa ndege, na marufuku ya safari za ndege kwa marufuku ya safari za ndege." Kwa mujibu wao, lengo ni kuilazimisha Saudi Arabia kusitisha mashambulizi na kuondoa mzingiro dhidi ya Yemen.
Wachangiaji wa mjadala huo walisema kuwa onyo lililotolewa kwa mashirika ya ndege kutotumia anga na viwanja vya ndege vya Saudi Arabia linaonyesha dhamira ya Sana'a ya kutekeleza kwa vitendo marufuku hiyo ya safari za ndege. Walisema pia kuwa kuhamisha uwanja wa mapambano hadi katika anga ya Saudi Arabia ni mabadiliko katika kanuni za mzozo na ni ujumbe kwamba kuendelea kwa hatua za kuongeza mvutano kutajibiwa kwa hatua zinazolingana hadi vita na mzingiro vitakapokoma.
Katika muktadha huo, Ali al-Qahoum, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah, alisema kuwa; misimamo inayoiunga mkono Saudi Arabia si jambo jipya, kwani wenye misimamo hiyo wamekuwa wakifuata mkondo huo tangu kuanza kwa mashambulizi na mzingiro wa Marekani, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu dhidi ya Yemen.
Aliongeza kuwa; misimamo hiyo yote imenunuliwa kwa fedha za Saudi Arabia na Falme za Kiarabu, na kwamba ni zao la mfumo wa kimataifa unaoongozwa na maslahi ya kifedha na unaofuata siasa za Kizayuni.
Kwa upande mwingine, Sheikh Hussein Hazib alisema kuwa; kama taarifa za Brigedia Yahya Saree zilizotolewa wakati wa kufungwa kwa Bahari Nyekundu kuelekea bandari ya Umm al-Rashrash zingerudiwa kwa kubadilishwa tu majina ya nchi na bandari kulingana na hatua ya sasa, jambo hilo lingeokoa muda na juhudi na pia lingekuwa ushindi.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, alisema hatua hiyo ingepelekea kutangazwa kwa mwisho wa vita na mzingiro, pamoja na kulipwa fidia na kutolewa kwa radhi. Pia alisisitiza kuwa; wananchi wa Yemen wana haki ya kufikiria zaidi ya chaguo moja la kujilinda katika nchi kavu na baharini.
Kwa upande wake, mshairi Yasin al-Farawi, katika shairi lake la lugha ya mazungumzo, alizungumzia maendeleo ya hivi karibuni na kusema kuwa; Mkuu wa Ujumbe wa Kitaifa wa Yemen, Mohammed Abdulsalam, amezima simu yake, jambo alilolitafsiri kuwa ni ishara ya kumalizika kwa hatua ya mazungumzo na majadiliano. Alisema kuwa kilichotokea katika Uwanja wa Ndege wa Abha ni hatua mpya katika kile alichokiita "mkakati wa kuvunja mzingiro."
Katika shairi hilo, lililochapishwa kwenye jukwaa la X, alisisitiza kuendelea kwa operesheni za kijeshi na kueleza kuwa marufuku ya safari za ndege ni sehemu ya jibu kwa kile alichokiita uchokozi. Pia alitoa wito wa kulengwa kwa viwanja vya ndege vya Saudi Arabia na kuyaonya mashirika yoyote ya ndege yatakayokiuka marufuku hiyo.
Naye mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Malik al-Madani alisema kuwa; jambo la kushangaza katika maendeleo ya hivi karibuni ni kutokuwepo kwa tamko lolote rasmi la kulaani operesheni ya makombora ya Yemen dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Abha.
Alisema kuwa; hakuna tamko lililotolewa na Falme za Kiarabu, Qatar, Bahrain, Marekani au mataifa mengine, akieleza hali hiyo kuwa ni mabadiliko makubwa katika medani ya kisiasa na hatua yenye athari kubwa kwa mustakabali wa Saudi Arabia katika eneo hilo.
Al-Madani pia alihoji iwapo Saudi Arabia imeanza kupoteza washirika wake na kubaki peke yake. Aliongeza kuwa tamko pekee rasmi lililotolewa lilikuwa la kulaani kulengwa kwa Uwanja wa Ndege wa Sana'a, ambalo lilitolewa na Iran, akisema kuwa hilo ni jambo la kipekee katika muktadha wa vita hivi.
Kwa mtazamo mwingine, mwanaharakati wa kijamii Sumayyah Asalah aliandika kuwa kushambuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Abha ni jibu la kushambuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Sana'a na vikosi vya Yemen vinavyoiunga mkono Saudi Arabia. Alihoji iwapo Saudi Arabia imeamua kuingia katika makabiliano ya moja kwa moja au kama Marekani inaishinikiza kujiingiza zaidi vitani ili kulinda maslahi yake na yale ya Israel.
Pia aliikosoa Saudi Arabia kwa sera zake katika miaka ya vita, akisema kuwa ilikosea kwa kutegemea migawanyiko kati ya nchi za Ghuba na kwa kutegemea makundi ya Kiislamu ya kisiasa, jambo ambalo, kwa maoni yake, linaifanya ipoteze washirika wake pamoja na uungwaji mkono wa wananchi wa Kiarabu.
Mwishoni, Mohammed al-Naw'ah, mwandishi wa habari wa televisheni ya Al-Masirah katika mkoa wa Al-Jawf, aliripoti kuwa; shughuli za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Abha zimesimama tangu saa 8:30 mchana. Alieleza kuwa safari nyingi za ndege zimefutwa na ndege ya mwisho iliyokuwa ikitoka Sharjah ilielekezwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Jeddah.
Alibainisha kuwa hali hiyo imejitokeza kufuatia kuongezeka kwa mvutano kati ya Sana'a na Riyadh, baada ya kulengwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a na baadaye kulengwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abha.
Maoni yako